Monday 28 October 2013



ALMAS ZA AFRIKA

 

UTANGULIZI

Almasi za Afrika ni diwani iliyoandikwa na Shabani Robert mwaka 1959 katika lugha ya Kiswahili na kuitafsiri katika lugha ya Kingereza kama African Diamonds. Kila shairi limetafsiriwa katika Lugha ya Kingereza kwa lengo la  kudhihirisha umahiri wake katika lugha hizi mbili, kuwasaidia wa geni wa utamaduni wa Kiswahili kuzifaidi almasi hizi adimu pamoja na kuonesha namna lugha ya Kiswahili isivyo maskini kama baadhi ya watu wanavyodhani na jinsi iwezavyo kuchukuana vyema na lugha nyingine za Kigeni hususani Kingereza. Tafsiri hizo siyo namna ya uandishi wa mashairi ya Kingereza. Hasha! Ushairi wa Kingereza una namna yake ya utunzi tofauti na namna ya utunzi wa ushairi wa Kiswahili. Kwa ufupi diwani hii inazungumzia maadili, utu wema, matendo mema, lugha ya Kiswahili, ujasiri na kujitoa mhanga. Kwa ujumla hizi ndizo Almasi zinazozungumziwa katika diwani hii yenye mkusanyiko wa mashairi kumi na moja ambayo ni Mtukufu Margaret, Wajibu wetu, Sahau,Rangi Zetu, Uzuri, Mali tulizo nazo, Kiswahili, Kiunzi chetu, Matendo, Tabia na Lugha. Shairi la Mtukufu Margaret limeandikwa na Mwidau Ulenge ndugu yake Shaban Robert kwa ajili ya kumkaribisha malkia wa Uingereza aliyezuru nchi ya Tanganyika mwaka 1959 wakati wa vuguvugu la ukombozi.



UCHAMBUZI WA FANI NA MAUDHUI

A.     MAUDHUI

Kwa mujibu wa Njogu na Chimera(1999) Maudhui ni ujumbe wa jumla kuhusu matukio kitu, wahusika au hali ya maisha kama yanavyojitokeza katika kazi ya fasihi, iwe riwaya, tamthiliya, shairi au wimbo.



1.      DHAMIRA

Wamitila(2004) anasema kuwa dhamira ni lengo la mtunzi katika utungo wake. Lengo hili hutokeza kwa wazo kuu ambalo hukuzwa katika utungo unaohusika kuanzia mwanzo mpaka mwisho.



Dhamira Kuu

Maadili mema na Maonyo katika Jamii



Dhamira Nyingine

i.                    Tabia Njema

Suala la tabia njema limekuwa likigusiwa na wandishi wengi. Katika Almasi za Afrika mwandishi anaeleza kuwa uzuri wa mtu hujenwa na tabia njema na siyo sura yake. Tabia ndiyo umfanya mtu akaheshimika au kudharaulika. Shairi la Tabia katika ubeti wa 3 linaelezea mawazo haya.



Tabia hupambanua,

Watu huwa mbalimbali,

Baadhi huchukuliwa,

Katika hadhi kamili,

We ni wa kivuli, hupita kama ruia.






Vilevile mwandishi anaeleza kuwa uzuri wa mtu siyo sura walas umbo lake bali ni tabia njema.Anaeleza haya katika shairi la uzuri.Ubeti wa 2.



Uzuri kupita huu,

Katika hii dunia,

Nawapa msisahau,

Ni uzuri wa tabia,

Ni johari ya heshima duniani kila mara.



ii.                  Matendo Mema

Mtu akiwa na matendo mema huheshimika katika jamii, hata akifa jamii yake huendelea kumbukwa na kumuenzi. Katika shairi la matendo ubeti wa 1 mwandishi anasema:



ROHO ivukapo ng’ambo yasaliayo matendo,

Mema yasiyo na Kombo hukumbukwa kwa matendo,

Mabaya yasiyo umbo huacha nyuma uvundo,

Matendo ni kumbukumbu ya mtu kukumbukwa.



iii.                Umuhimu wa Lugha

Shaban Robert anasema kuwa kila lugha kote duniani ni bora na ina manufaa kwa waitumiao kwa hiyo anasisitiza kutodharau lugha ya mtu mwingine. Anaendelea kusema kuwa mtu asiye na lugha ni sawa na mtumwa maana hata wanyama wa porini wana lugha zao wanazozitumia kuwasiliana.Katika sairi la Lugha Ubeti 2 anasema:



Kila lugha ni dhahabu, hazina bora upeo,

Ni mali ya kuhesabu, kila siku uishiyo,

Lugha haina aibu, ni maumbile unayo,

Tena kitu maabuu, Katika mali za leo,

Hasa wastaarabu, kutumia wajuao,

Kwao lugha ni kitabu, elimu na ufunuo.



Vilevile lugha ni mali ya asili, ni tamu kwa waitumiao na ni cheo kwa mtu aitumiaye lugha husika.Ubeti wa 6 mwandishi anasema:



Kila lugha huwa mali, usijali wabezao,

Mali yenyewe halali, kila mtu kuwa nayo,

Lugha mali ya asili, mtu huzaliwa nayo,

Wala haina badili, kwa mtu kama anayo,

Lugha isipokubali, na akili kwenda nayo,

Maneno yako batili, awafaamu wenzio.

iv.                Umuhimu wa Lugha ya Kiswahili

Shaban Robert ni mmoja wa watetezi wa lugha ya Kiswahili. Katika hii anawaasa wanajamii kukipa kukipa hadhi Kiswahili kwani ndiyo lugha mama, nyingine hazitatufaaa kwani ni za kuazima. Katika shairi la Kiswahili ubeti wa 8 mwandishi anasema:



            Kila mtu lugha yake, ndiyo mtumishi mwema,

            Lugha nyingine makeke, kwa nahau kuzisema,

            Kila mkuu na pake, hana hadhi akihama,

            Na Kiswahili nivike, joho lako la heshima,

Titile mama li tamu, njingine haliishi hamu.



Hata hivyo Shaban Robert anatambua umuhimu wa blugha za kigeni hasa kujipatia maarifa. Anabainisha hayo katika shairi la Kiswahili ubeti wa 14.



            Lugha ngeni ni elimu, hili sana naelewa,

            Sitishiwi na ngumu, kwa kujifunza najua,

            Lakini ilivyo tamu, lugha ya kulelewa,

            Kusema yanilazimu, kwa hali yoyote kuwa,

            Titile mama li tamu, jingine haliishi hamu.



v.                  Suala la Elimu

Mwandishi anasisitiza elimu kama njia ya kumkomboa mwanadamu katika hali zote za maisha ukiwemo unyonyaji wa kikoloni. Mwandishi katika shairi la mali tulizo nazo ubeti wa 7 anasema:

            Tuna vyuo vya elimu, huenda tukakariri,

Maji ya kunywa matamu huburudisha sudari,

Akili zetu timamu afya haina dosari,

Bali wachache wa ahmu wa tendo la ujasiri.



Vilevile mwandishi anaona kuwa kujifunza lugha ngeni pia ni njia ya kujipatia elimu. Shairi la Kiswahili ubeti wa 14 linadokeza:

            Lugha ngeni ni elimu, hili sana naelewa,

            Sitishiwi na ngumu, kwa kujifunza najua,

            Lakini ilivyo tamu, lugha ya kulelewa,

            Kusema yanilazimu, kwa hali yoyote kuwa,

            Titile mama li tamu, jingine haliishi hamu.




vi.                Ujasiri na Kujitoa Mhanga

Mwandishi anawahimiza watu kuwa na roho  ya ujasiri na kujitoa mhanga ili kujikomboa dhidi ya madhila ya kijamii kama vile unyonyaji wa kikoloni. Anahimiza hayo katika shairi la Mali tulizo nazo ubeti wa 10 na 12.





            10.       Bila matendo aushi, haja zetu hazijiri,

                        Dunia tunayoishi, hata kitu cha hiari,
                        Hupata kwa ushawishi, na bidii na dhamiri,
Hatupati kwa utashi, usio na ujasiri.


            12.       Haipatikani kitu, kama sisi si tayari,

                        Kutenda wajibu wetu, kwa bidii na kwa ari,

                        Kushawishi haja zetu, mpaka zikatukiri,

                        Na hupata kila kitu, kama tuna ujasiri.



vii.              Ubaguzi wa Rangi

Mwandishi anawakemea watu wenye tabia ya kubaguana wenyewe kwa wenyewe na kuhukumiana kwa kigezo cha rangi. Anasema kuwa rangi si uchafu, si dalili ya machungu, dhambi, mapungufu wala kashfa bali nip ambo la Mungu. Shairi la Rangi Zetu Ubeti wa 2 na 3.



2.      Hupamba nyota na mbingu, na mawaridi nma afu,

Rangi adhama ya Mungu, na mwilini si uchafu,

Si dalili ya machungu, dhambi wala upungufu,

Rangi heba yake Mungu, Mwenyezi mkamilifu.



3.      Ni urembo wake Mungu, Mwenye miliki ya sifa,

Napambo lamalimwengu, shahada ya taarifa,

Wajinga wa ulimwengu, rangi hudhani kashfa,

Rangi pambo lake Mungu, si alama ya maafa.



viii.             Dini

Mwandishi anawakumbusha watu kumtumainia Mungu kwani yeye ndiye muumbaji wa vitu vyote na alitakali liwe huwa. Maisha ya mwanadamu yapo kutokana na matakwa ya Mungu kwani yeye huweza kulifanya fupi kuwa refu. Shairi la Rangi Zetu ubeti wa 4 na 6.



Ubeti wa 4.      Twajua mwenyezi Mungu, kwa mambo mabadilifu,

Shani zake na mizungu, ni Bwana wa masanifu,

La ardhi na la mbingu, neno lake husadifu,

Rangi heba yake Mungu, mwenyezi mkamilifu.



Ubeti wa 6.      Hashindwi mwenyezi Mungu, fupi kulipa refu,

Hashindwi na malimwengu, watawaliwa na utu,

Hashindwi katika mbingu, kwa rain a utukufu

Rangi heba yake Mungu, mwenyezi mkamilifu

4.      UJUMBE

Wamitila(2004) anaeleza kuwa ujumbe ni dhana ituwayo kuelezea taarifa ambazo msanii au mtunzi hukusudia kuzifikisha kwa wasomaji wake au hadhira yake kama njia mojawapo ya kuhakikiha kwamba dhamira yake imetimia. Ni mafunzo yanayopatikana ndani ya kazi ya fasihi. Katika diwani hii ujumbe mbalimbali umejitokeza.



v  Uzuri wa mtu siyo umbo wala sura yake bali ni tabia. Shairi la Uzuri

v  Elimu ni msingi wa maendeleo katika jamii yoyote. Shairi la Mali tulizo nazo.

v  Ubaguzi wa Rangi haufai. Shairi la Rangi zetu.

v  Tuthamini lugha yetu ya Kiswahili. Shairi la Kiswahili.

v  Ujasiri na kujitoa mhanga ni chachu ya maendeleo. Shairi la Mali Tulizo Nazo.
v  Tuzithamini lugha ngeni, tujifunze ili kuongeza maarifa lakini tusizitupe lugha zetu. Shairi la Kiswahili.

v  Kusamehe na kusahau mabaya tuliyotendewa ni muhimu. Shairi la Sahau.
5.      MIGOGORO

Kwa kiasi kikubwa migogoro iliyojitokeza katika diwani hii ni ile inayomhusu mshairi mwenyewe dhidi ya  hadhira anayoiandikia. Ni baada ya kuchukizwa na mwenendo wa jamii ukajengeka mgogoro katika nafsi yake na kuamua kuandika akiihasa jamii kuachana na matendo maovu, tabia mbaya, chuki na woga.



6.      MTAZAMO

Kwa mujibu wa Wamitila(2004) mtazamo ni namna au jinsi mtu anavyoyachukulia mambo au anavyofikiri juu ya jambo Fulani. Kuna mtazamo wa kimapokeo na wa kimapinduzi. Katika diwani hii mtazamo wa mwandishi ni wa kimapinduzi kwani ameeleza mambo anuai kama ujasiri, elimu na kujitoa mhanga ambayo ni mambo muhimu kwa jamii ili kujikomboa na adha za maisha.



7.      MSIMAMO

Ni hali ya mtunzi kushikilia jambo Fulani kuwa ni sahihi hata kama jamii nzima ahikubaliani nalo. Upo msimamo wa kidhanifu na wa kiyakinifu. Katika diwani hii mwandishi anaonekana kuwa na msimamo wa kiyakinifu. Msimamo huu umejibainisha katika mashairi ya Rangi, Kiswahili na Mali tulizo nazo.



8.      FALSAFA

Wamitila(2004) anaeleza kuwa falsafa ni mawazo aliyo nayo mwandishi juu ya maisha ambayo hujitokeza katika maandishi yake. Mawazo hayo anayaamini na kuyashikilia kama ukweli unaoongoza maisha yake na ya jamii kwa ujumla. Katika diwani hii mwandishi amejenga falsafa yake juu ya wema katika maisha kama ndio msingi wa maisha bora miongoni mwa wanadamu. Falsafa hii inajidhihirisha katika mashairi ya Wajibu wetu, saahu, Rangi zetu, Tabia na Matendo.





B.      FANI

Kwa mujibu wa Senkoro(1982) fani ni ufundi wa kisanaa anaoutumia msanii katika kazi yake.



1.      WAUSIKA

Baadhi ya wahusika aliowatumia msanii katika kazi hii ni hawa wafuatao:

i.                    Malkia Margaret. Shairi la Mtukufu Margaret

ii.                  Wamasai, Wambulu, Waha na Wamakonde. Shairi la Lugha.

iii.                Mama. Shairi la Kiswahili.

iv.                 Gavana. Shairi la Mtukufu Margaret.

  
2.      MUKTADHA

Mandhari ya diwani hii ni nchini Tanganyika kipindi cha utawala wa Waingereza. Harakati za kupigania uhuru zilikuwa zimeshtadi.




3.      MUUNDO

Senkoro(1982) anaeleza kuwa muundo ni mpangilio na mtiririko wa kazi hiyo kwa upande wa visa na matukio. Katika ushairi muundo unahusisha idadi ya mistari, vipande au mishororo, beti, urari wa vina na mizani pamoja na kibwagizo.



i.                    Idadi ya Mishororo

a)      Tarbia(Mishororo 4): Mashairi la Mtukufu Margaret, Sahau, Rangi Zetu, Mali tulizo nazo

                                       na Matendo.


b)     Takhmisa(Mishororo 5): Mashairi ya Uzuri, Kiswahili na Tabia.



c)      Usita(Mishororo 6): Shairi la Wajibu Wetu.





ii.                  Idadi ya Beti

a)      Beti 32: Shairi la Mtukufu Margaret. Uk. 4-18



b)     Beti 31: Shairi la Kiswahili. Uk. 42



c)      Beti 14: Shairi la Mali Tulizo Nazo. Uk. 36 na Rangi Zetu. Uk. 30



d)     Beti 12: Shairi la Lugha. Uk. 70



e)      Beti 8: Shairi la Matendo. Uk. 64



f)       Beti 5: Shairi la Tabia. Uk. 68 na Uzuri Uk. 28



g)      Beti 4: Shairi la Kiunzi Chetu. Uk. 62



h)     Beti 2: Shairi la Wajibu Wetu. Uk. 20



iii.                Urari wa Vina na Mizani

Katika mashairi ya Mtukufu Margaret, Sahau, Rangi Zetu, Mali Tulizo Nazo na Matendo vina vya kati na vya mwisho vinafanana kwa kila shairi. Idadi ya mizani ni 16 kwa kila mshororo.




iv.                Kibwagizo

Mshairi ametumia vina vya aina mbili. Kibwagizo cha kawaida na Kinabahari.



a)      Kibwagizo cha Kawaida

Kibwagizo cha namna hii hubadilika badilika kila ubeti. Katika diwani hii kina cha namna hii kimetumiwa katika mashairi ya Mali Tulizo Nazo Uk. 36, Wajibu Wetu Uk. 20, Uzuri Uk. 28, Tabia na Lugha.



b)     Kinabahari

Hiki hakibadiliki, ni kilekile tangu ubeti wa Kwanza mpaka wa Mwisho. Kibwagizo cha namna hii kimejitokeza katika mashairi ya Matendo Uk. 64, Kiswahili Uk. 42 na Mtukufu Margaret Uk. 4





4.      MTINDO

Kwa mujibu wa Njogu na Chimera(1999) mtindo ni tabia ya utungaji inayompambanua mtunzi mmoja na mwingine. Mitindo iliyotumika katika diwani hii ni hii ifuatayo:



i)                    Mtindo wa Kimapokeo

Hii ni aina ya utunzi wa mashairi yenye kutii sheria za utunzi wa mashairi kama vile urari wa vina na mizani, mishororo mine katika ubeti na kibwagizo aghalabu kinabahari. Kwa kiwango kikubwa mwandishi wa diwani hii ametumia mtindo wa kimapokeo. Mashairi kama Mtukufu Margaret, Sahau, Rangi zetu, Mali tulizo nazo na Matendo yote yametii kanuni hii ya uandishi.



ii)                  Mtindo wa Kisasa

Mtindo wa aina hii hautii sheria za utunzi kama zilizoelezwa hapo juu. Mashairi yaliyofuata mtindo huu katika diwani ya Almasi za Afrika ni Wajibu wetu na Uzuri.



iii)                Mtindo wa Kutumia Herufi Kubwa

Mbinu Hii imetumika kwa neno la kwanza la mshororo wa kwanza kwa kila ubeti wa kwanza katika mashairi yote kumi na moja.




iv)                Mbinu ya Mchezo wa Maneno

Mbinu hii imetumika kwa madhumuni ya kufafanua kile kinachosemwa kwa kuongeza vionmjo. Mbinu hii imetumika katuka shairi la Kiswahili.



            Mfano wa neno jambo, mkato wa una jambo,

            Jawabu lake sijambo, tafsiri sina jambo,

            Tazameni hili pambo, lizidishavyo urembo,

            Wa kuuliza sana mambo, kwa usemi wenye umbo,

            Titile mama li tamu, jingine haliishi hamu.





5.      MATUMIZI YA LUGHA

Kwa ujumla mshairi ametumia lugha nyepesi na ya kueleweka kwa wasomaji.



i.                    Matumizi ya Methali

a)      Mtenda mema duniani, zawadi yake ni thawabu. Shairi la Kiswahili.

b)      Bila matendo aushi haja zetu hazijiri. Shairi la Mali tulizo nazo.

c)      Titi la mama ni tamu hata kama la mbwa. Shairi la Kiswahili.


ii.                  Matumizi ya Tafsiri

Mashairi yote kumi na moja yametafsiriwa katika lugha ya Kingereza ili kupanua wigo wa hadhira, ili hata hadhira isiyofahahamu Kiswahili mwisho wa mwisho iweze kunufaika na Almasi hizi adhimu. Pia mshairi alitaka kudhihirisha mwingiliano uliopo baina ya Kiswahili na lugha ngeni hususani Kingereza.



iii.                Tamathali za Semi

a)      Tashbiha

Wamitila(2004) anaeleza kuwa tashbiha ni ulinganisgi wa moja kwa moja na gutambulisgwa kwa viunganishi kama, mithili, mithili ya..,sawa na……nk.

Ktika diwani hii tashbiha zimejitokeza zaidi katika shairi la Sahau.



            Ni njema kama dhahabu tabia ya kusahau.



Pia katika shairi la Tabia

            Humea kwa kupendeza kama yenye manukato,

            Humea kwa kuchukiza kama madhambi.

           



b)     Sitiari

Msokile(1993) anaeleza kuwa sitiari ni tamathali ya usemi ambayo kwa kawaida huhusisha matendo, kitu au tabia ya vitu vyenye maumbile tofauti. Ulinganisho huu unahusisha misingi au sifa zinazopatikana katika vitu vyote viwili ingawa sifa hizo haziwi wazi kati ya kitu na kitu.

Katika diwani hii Sitiari zimetumika katika shairi la Sahau.



            Sahau kwetu dhahabu tena ni kitu kikuu,

            Kumbukumbu ni wajibu, na faraja ni sahau,

            Mashaka yanapoghibu, roho zinakwenda juu,

            Faraja kubwa ajabu, kwa mtu ni kusahau.



c)      Tashhisi

Mulokozi(1996) anaeleza kwamba hii ni tamathali ya kukipa uhai na tabia za kibinadamu kitu ambacho hakina uhai au tabia hizo.

Mifano ya tashhisi zilizotumika katika diwani hii ni katika shairi la Kiswahili.



            Kiswahili kikikopa, na lugha nyingine pia,

            Ambazo zimenenepa, jambo hili hutumia,

            Ama sivyo zingetupwa, kwa kukosa manufaa,

            Kiswahili kikikopa, si hila ndiyo tabia,

            Titile mama li tamu, jingine haliishi hamu.



d)     Takriri

Takriri ni mrudiorudio wa neno au wazo Fulani kwa lengo la kuweka msisitizo. Katika shairi la Lugha mwandishi ametumia takriri.



Haihati, haihati…



e)      Nidaa

Msokile(1993) anasema kuwa nidaa ni msemo ambao unaonesha kushangazwa kwa jambo Fulani. Huambatana na alama ya mshangao kukubali jambo, kuchukia ama kuonesha heshima kuu. Nidaa zilizotumika katika diwani hii zinapatikana hasa katika shairi la sahau:



            Mangapi ya kuhesabu hapa chini licha juu!

            Ya hatia na thawabu na dhuluma na dharau!

            Afadhali kuwa bubu au ndani ya sahahu!

            Faraja kubwa ajabu kwa mtu ni kusahau!







iv.                Ishara na Taswira

Taswira hurejelea picha ijengekayo akilini mwa msomaji kutokana na athali za matumizi ya lugha katika kazi ya fasihi. Hugusa hisia za ndani za msomaji na kumfanya achukie,kupenda, kukasirika, kucheka, kupata kichefuchefu na ahta kuogopa. Baadhi ya taswira zilizotumika ni:



a)      Almasi

Ni madini ghali na adimu. Katika diwani hili limetumika kitaswira kumaanisha tabia njema, matendo mema, Lugha ya Kiswahili, ujasiri na kujitoa mhanga ambavyo kimsingi vinapendwa katika ustawi wa jamii bora kama yalivyo madini ya almasi.



b)     Titi la mama ni tamu hata kama la mbwa. Shairi la Kiswahili.

Titi la mbwa halipendwi na binadamu, siyo tamu kwa binadamu ila ni tamu sana kwa watoto wa mbwa. Mwandishi ametumia taswira hii kuihimiza jamii ya waswahili umuhimu wa kuithamini lugha ya Kiswahili licha ya kwamba wengine wasiojua utamu wake wanaweza kuwa wanaibeza.






KUFAULU NA KUTOKUFAULU KWA MWANDISHI

KIFANI

Mwandishi amefaulu katika matumizi ya mtindo, muundo na matumizi ya lugha nyepesi yenye kueleweka vema kwa hadhira pana ikichagizwa na tafsiri ya Kingereza. Vipengele vya fasihi ya Kijadi vimehusishwa kama methali na misemo ili kudhihirisha uhalisia wa fasihi ya mwafrika.



KIMAUDHUI

Mwandishi amefaulu kwa kiasi kikubwa kuifikishia hadhira yake ujumbe ambao ni fawafu katika maisha ya kila siku kwa njia ya ushairi.




JINA LA KITABU

Almasi ni madini yenye thamani kubwa yanayopatikana kwa baadhi ya maeneo hapa Afrika. Yanatamanika kwa watu wengi wenye kutambua thamani yake. Kwa kutumia madini haya historia ya mtu binafsi hata taifa au mataifa huweza kubadilika haraka sana kutoka hali duni kwenda hali bora kabisa. Sifa hizo za Almasi ni sawa na zile za lugha yetu ya Kiswahili inayoongelewa katika maeneo mengi hapa barani Afrika. Vilevile tabia njema, utu wema, upole, unyenyekevu, kusameheana na kusahau mabaya tuliyotendewa vyote hivi hujenga utu wa mwafrika na kulinganishwa thamani yake na madini ya Almasi. Hivyo basi kwa muktadha huu jina  Almasi za Afrika linasadifu yote yaliyomo ndani ya kitabu.



HITIMISHO

Kwa hakika diwani hii ni kurunzi fawafu ya kuyamulika mapito ya hadhira ya mwandishi wa diwani hii ambayo ni Tanzania ya sasa na Afrika kwa ujumla. Ni diwani iliyoshiba kwa wingi na uzito wa maadili, maonyo na umuhimu wa mambo anuai ambayo mahenga ameikirimia hadhira yake. Hivyo hii ni diwani bora.











MAREJEO



Msokile, M.(1993) Misingi ya Uhakiki wa Fasihi. Dar es Salaam, EAEP



Mulokozi, M.M.(1996) Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam, TUKI



Njogu, K. na R. Chimera(1999) Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu.

                                                        Nairobi, Kiswahili Tertiary Publishing Project.

Robert, S.(1959) Almasi za Afrika. London, Nelson.



Senkoro, F.E.M.K.(1982) Fasihi. Dar es Salaam, DUP



Wamitila,K.W.(2004) Kichocheo cha Fasihi:Simulizi na Andishi. Nairobi, Focus Publications Ltd