Monday 12 August 2013



                                          Mofim ni nini?

 Neno mofimu ni neno pana ambalo wataalam mbalimbali wamekuwa na mawazo mbalimbali katika kueleza maana yake.Wafuatao ni baadhi tu ya wataalam walioeleza maana ya mofimu.

Massamba na wenzake (1999) uk 36 wanasema kuwa,Mofimu ni kipashio kidogo amilifu katika maumbo ya maneno.Hapa kipashio kina maana ya umbo la neno au umbo katika neno lisiloweza kugawanyika katika sehemu nyingine ndogo zaidi.

Ruth Mfumbwa Besha (1994),anafafanua kuwa Mofimu ni vipashio vinavyoonesha uhusiano uliopo kati ya sauti za msingi za lugha (fonimu) na maana maalum katika sarufi ya lugha.

Pia John Habwe na Peter Karanja (2004),wamemnukuu Hartman (1972) katika kitabu chake kuwa,mofimu ni dhana ya kidhahania iliyomo akilini mwa mtu na sehemu ya umilisi wa mzawa wa lugha husika na anaendelea kusema kuwa hii hudhihirika kiutendaji ama kimaandishi au kimatamshi.

Vilevile Massamba na wenzake katika kitabu chao cha Sarufi Miundo Ya Kiswahili Sanifu wanasema Mofimu ni kipashio kidogo kabisa chenye uamilifu wa maana katika maumbo ya maneno.

Assumpta K.Mtei naye anasema kuwa,Mofimu ni kipashio kidogo kabisa dhahania cha lugha chenye maana.Tunasema kipashio dhahania kwa sababu hakionekani wala haiwasilishwi kupitia uandishi imo akilini mwa msemaji.

Kwa mujibu wa James Salehe Mdee(1988) ametoa aina  mbili za mofimu ambazo ni, Mofimu huru na Mofimu tegemezi ambapo, Mofimu huru ni mofimu inayoweza kusimama peke yake na kuweza kutumiwa katika tungo bila kuwa na kiambishi chochote . Mofimu huru zina hadhi ya neno na zinaweza kuwa aina yoyote ya neno kama vile nomino,kitenzi ama kiwakilishi.

Licha ya wataalamu mbalimabili tulio waangalia katika kutoa maana ya mofimu, sisi wanazuoni wachanga tumeona kuwa”Mofimu ni kipashio kidogo cha lugha chenye maana kisarufi na kileksika” mfano kitenzi “anacheza” kinaweza kubainishwa na kuleta maana kisarufi yaani;



Baada ya kangalia maana mbalimbali kuhusu mofimu tunawe kutumia mifano michache kubainisha mofimu katika maumbo yafuatayo: Pendezesha, Chomelea, Usawazisho, Myeyusho, Bahatinasibu, Waogeleaji, Makumbusho, Msongamano, Usawazisho, Waogeleaji, Maombezi.

A-        ni kiambishi awali nafsi ya pili umoja
-na-      ni kiambishi cha njeo cha wakati uliopo
-chez-   ni mzizi wa kitenzi
              -a-       kiambishi tamati maana

Kwa upande mwingine mofimu inaweza kuwa na maana ya kileksika mfano, maneno kama baba,mama,shangazi na mengineyo yanatupa maana moja kwa moja kikamusi, kiundani maneno hayo ndiyo tunayoweza kuyaita mofinu huru ambazo zikisimama peke yeke zinaleta maana na haziwezi kugawika zaidi.

Maumbo mbalimbili ya mofimu katika lugha ya Kiswahili na hata lugha nyingine huwa na maana na pia uhusiano wa vipashio ili kujenga maana sahihi iliyo kusudiwa katika maneno husika. Maumbo na uhusiano huo usipozingatiwa huweza hata kuathiri maana ya neno. Kwa hiyo uhusiano na mpangilio wa maumbo ya vipashio katika lugha ya Kiswahili ndio unaoweza kuleta maana zilizokusudiwa katika maneno.

Maumbo yafuatayo ya Kiswahili yamebainishwa mofimu zake na kuelezea uhusiono wa vipashio vinavyohusika.

(a) Pendezesha

 -Pend-   mzizi wa neno

 -ez-        kiambishi cha usababishi

 -esh-      kiambishi cha utendeshi

  -a-         kiambishi tamati maana

(b) Chomelea

-chom-   mzizi wa neno

-e-          kiambishi nyambulishi cha utendea

-le-        kiambishi kinachoonyesha ukubwa wa tendo (linafanywa mara nyingi)

-a-          kiambishi tamati

(c) Usawazisho

-u-           kiambishi awali kinominishi

-sawa-     mzizi wa neno

-z-            kiambishi cha usababisho

-ish-         kiambishi cha usababisho

-o-            kiambishi tamati kinominishi

(d) Myeyusho

-m-     kiambishi awali kinominishi

-yeyu-  mzizi wa neno

-sh-       kiambishi cha usababishi

-o-         kiambishi tamati kinominishi



(e) Bahatinasibu

Hii ni mofimu huru ambayo imeundwa na mofimu mbili zenye maana tofauti ambapo zikiwekwa pamoja tunapata maana sahii iliyopo kwenye umbo letu(neno).

Kutofuata mpangilio na uhusiano wa mofimu hizo hautaleta maana iliyokusuduwa katika umbo hilo, mfano neno hilo likigeuzwa na kuwa nasibubahati hatutapata maana iliyokusudiwa. Kutokana na umbo hilo kila mofimu ikisimama peke yake yaani nasibu na bahati tunaweza kupata maana hivyo neno Bahati nasibu ni neno huru ambalo haliwezi kugawanyika.

(f) Waogeleaji

-wa-   kiambishi awali cha ngeli ya kwanza uwingi

-og-   ni mzizi wa neno

-e-     kiambishi cha utendea

-le-    kiambishi kinachoonyesha kiwango cha ukubwa wa tendo

-a-     kiambishi tamati kijenzi

-ji-    kiambishi tamati kinacho onyesha ujirudiajirudiaji wa tendo.
(g) Makumbusho

-ma-        kiambishi kinominishi cha mahali

-kumbu- mzizi wa neno

-sh-         kiambishi kitendeshi au kisababishi

-o-           kiambishi tamati kinominishi.

(h) Msongamano

-m-       kiambishi awali kinominishi

-song-  mzizi wa neno

-am-     kiambishi cha uambatani (kiambishi tamati cha mwambatano)

-an-      kiambishi cha utendano

-o-        kiambishi kinominishi.

(i) Maombezi

-ma-    kiambishi awali cha ngeli ya wingi

-omb-  mzizi wa neno

-ez-      kimbishi tamati kitendeshi (-e- kiambishi cha utendea)

-i-         kiambishi tamati kinominishi (-zi- kiambishi kinominishi)

Kwa kuhitimishi ni kwamba kutokana na ubainishaji huo wa mofimu na uhusiano wake ni dhahiri kuwa uhusiano wa vipashio hutegemea mpangilio wa vipashio hivyo, yaani nafasi ya mofimu katika neno. Na kila mofimu ina kazi yake kutegemea mpangilio uliopo katika neno hilo.







MAREJEO

Besha,R.M (1994), Utangulizi wa Lugha na Isimu. Dar es salaam.DUP ltd.

Habwe,J na P.Karanje (2004), Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi. Printpak ltd

Kihore,Y.M na wenzake (2001), Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu.

                                         Dar es salaam. TUKI.

Matei,A.K (2008), Darubini ya Sarufi. Nairobi.Acme Press.

Massamba D.P.B na wenzake (1999), Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu.

                                                       Dar es salaam.TUKI.

Mdee, J.S (1988), Sarufi ya Kiswahili. Dar es salaam. DUP ltd.