FASIHI

                        FASIHI YA WATOTO NA VIJANA.

Historia ya maendeleo ya  fasihi ya watoto kwa ujumla imegubikwa na matatizo lukuki nchini Tanzania. Jadili kauli hii ukianza kujikuta katika mawanda mapana na mafupi halafu upendekeze njia za kutatua matatizo haya.
hili ni swali la semina lililotolewa kwa kila mmoja atafakari na kutoa msimamo wake. hii ndiyo ilikuwa tafakari yangu.


 

Katika kujibu swali hili nitaangalia maana za istilahi zilizotumika katika sawali kisah nitaangalia katika mawanda mapana yaani nitaangalia maendeleo ya fasihi ya watoto na viijana katika mataifa ya nje ya  Afrika na baadae nitaangalia historia ya maendeleo ya fasihi ya watoto na vijana Tanzania kisha matatizo yanayoikumba fasihi hii, njia za kutatua matatizo na baadae hitimisho na marejeo.
Women’s Aid collective (2002) wakilejerea baadhi ya fasili zilizotolewa na watoto wenyewe na sheria za watoto wanafasili mtoto kuwa ni mtu mwenye umri wa chini ya miaka 14 na mtoto mdogo ni mtu mwenye umri wa miaka 14 lakini ambaye hajatimiza miaka 17. Katika fasili hii watalamu hawa wanajaribu kuibua tofauti kati ya mtoto na mtoto mchanga.
TUKI (2004) Mtoto ni mtu mwenye uri mdogo. Tuki hawafafanui umri mdogo ni upi.
 Young Adult Library Service Assciation (YALISA) (2011) wanatoa fasili ya kijana kuwa ni mtu mwenye umri wa miaka 12 hadi 18. Wanaendelea kusema kuwa wasomaji wa fasihi nao walitoa fasili ya vijana na wa toto fasili ambayo imefanana na fasili hii iliyotolewa na (YALISA) pia wanaendelea kusema kuwa fasili ya vijana na watoto haikutolewa na hao tu bali hata wachapishaji wa vitabu vya fasihi nao walitoa fasili yao kuwa “ vijana ni watu wenye umri kuanzia mikaka 10 hadi 25.
TUKI (2004) Kijana ni mwana mdogo, mtoto wa kiume au wa kike hadi kubalehe.
 Tukilejerea maana ya fasili zilizotolewa kuhusu watoto na vijana ni dhahili kwamba zinaibua utata katika kujua kijana ni yupi na mtoto ni yupi. Kwani tunaona fasili ya kuwa kijana anaweza kuanzia miaka 10 hadi kufikia miaka 25, wakati wengine wanachukulia kipindi cha miaka 10 kama kipindi cha utoto. Hivyo nanaweza kuhitimisha hoja hii kwa kusema kuwa suala la mtoto na kijana ni yupi bado linaleta utata katika kufasili dhana hizo. Baada ya kuangalia maana ya watoto na vijana sasa tuangalie maana ya fasihi ya watoto na vijana.
Fasihi ya watoto na vijana Irene (2003) akinukuliwa na Bruno(2011) anasema kuwa fasihi ya watoto na vijana ni fasihi iliyoandikwa hasa kwa ajili ya jinsia ya kiume. Ansema fasihi hii
                                                                          1.

ilijihusisha na masula ya michezo, usakaji au usakaji ambao uliishia na ushindi pia zilihusu
habari za kuvutia pamoja na hadithi za kisayansi. Anaendelea kusema kua ukuaji na uendeleaji wa fasihi hii ya watoto na vijana ulisaidiwa na kuibuka kwa uhapishaji wa magazeti yaliyouzwa kwa bei lahisi huenda na fasihi za watoto ziliandikwa katika magazeti hayo. Fasili hii inaibua mawazo kuwa huenda jinsia ya kike haikupea nafasi kipindi cha zamani huko Amerika. Lakini  tunaweza kufasili fasihi ya watoto na vijana kuwa ni kazi ya sanaa inayotumia lugha kufikisha njumbe kwa jamii inayohuska hasa watoto na vijana.
Baada ya kuangalia fasili hizo sasa hatuna budi kuangalia histori ya maendeleo ya fasihi ya watoto na vijana kwa kuanza kujikita katika mawanda mapana na kumalizia na mawanda mafupi. Kwa kuanza na mawanda mapana yaani katika nchi za nje ya Afrika fasihi ya watoto na vijana inaonekana kuwa  ilianza zamani kidogo kuliko katika Tanzania na afrika kwa uliandika bila kuzingatia watoto wala vijanajumla.
Kwa mjujibu wa Michael Cart (2005) akinukuliwa na Bruno (2011) anasema kabla ya kipindi cha kuanguka kwa soko la dunia haikuwepo dhana ya kuangalia watoto au vijana katika jamii. Waandishi waandishi waliandika bila kujali uwepo wa makundi hayo yaani ya watoto na vijana. Lakini pamoja na hayo anasema kuwa hakuna mwenye uhakika lini haswa fasihi ya kwanza ya watoto na vijana iliandikwa. Kwani Kate Angew(2001) na Maureen Nimona(2001)  katika Bruno (2011) wanasema fasihi ya kwanza kuhusu watoto iliandikwa (1956) wakati Michaeli Cart (keshatjwa) anasema kuwa riwaya ya “the outsiders” ya S.E Hintons iliyochapishwa mwaka (1967) ndiyo inasemekana kuwa ya kwanza. Kufikia miaka ya (1970)na (1980) wachapishaji walianza kujua mchango wa vijana katika soko la uuzaji wa vitabu vya fasihi hasa ya vijana. Waandishi wengi walianza kuandika kwa kuwavutia vijana kwa kutumia picha nzuri katika majarida ya vitabu pamoja na kutumia maelzo ya muhutasari nyuma ya vitabu vyao ili kuwavutia wasomaji. Angrew (2001) na Nimon(2001)  katika Bruno (2011).
Miaka ya (1990) waandihsi wa fasihi walijikuta wakiandika zaidi fasihi ya  vijana kwani kipindi hicho vijana walikuwa na mwamko wa usomaji sana kutokana na elimu waliyokuwa wanapata
                                                                             2.
na ussomaji huo uliweka ulileta mwachano kati ya watoto na vijana. Cart.  keshatajwa.  Kufikia miaka ya (2000) waandishi wengi walijirudi na kuanza kuadika kwa kuzingatia hadhira husika.
Baada ya mwaka (2000) fasihi iliyofuatia iliitwa fasihi ya kisasa, kwa mujibu wa Holly Koelling ambaye ni mhakiki wa kitabu cha “The Best Book for Young Adults (2007) katika Bruno, anasema kuanzia kipindi cha  (2000 – 2006) kulikuwa na makala zilizochapishwa kwa ajili ya vijana zilikuwa 577. Anasema machapisho haya yalihusisha mashairi, hadithi za kubuni,  fantasia na nyingine nyingi. Cart ansema fasihi ya vijana wa leo ni fasihi ambayo inahusu masuala ya kisasa au kileo yanayohusu uhalisia wa vijana huko Amerika.
Baada ya kuitalii na kuiona historia ya fasihi ya watoto na vijana katika mawanda mapana sasa tuangalie historia ya maendeleo ya fasihi ya watoto na vijana katika mawanda mafupi yaani kwa kujikita katika Tanzania. Historia ya maendeleo ya fasihi ya watoto na vijana Tanzania tunaweza kuiangalia kuanzia kipindi kabla ya ukoloni hadi hivi leo. Kabla ya ukoloni inasemekana kulikuwa na njia moja ya usimuliaji kwa mujibuwa mwandishi wa kitabu cha Kateta mwana Charo (1976) anasema;
                               “Usimulizi wa hadithi ilikuwa ndiyo njia ya pekee
                                 iliyotumiwa kwa kutolea elimu kabla mataifa ya kigeni
                                 hayajavamia Afrika. Waliopewa jukumu hili walikuwa wazee…”
 na kipindi cha ukoloni fasihi ya watoto na vijana haikuwepo tunaona fasihi zilizokuwepo zilihusu masuala mbalimbali mfano utumwa,  riwaya  Uhuru wa watumwa ya James Mbotela (1934), katika kipindi chote cha wageni kutoka nje au wakoloni  bado Tanzania hapakuwa na fasihi za watoto na vijana. Hadi kufikia miaka ya (1950-1960) na kuendelea kulikuwa waandishi waandishi wa vitabu vya fasihi lakini  hikuwepo fasihi ya watoto na vijana. Mfano fasihi za Shaaba Robert kama Kufikirika, na Diwani ya Shaabani Masomo yenye adili(1959) na kuanzia miaka ya (1970) kulikuwa na fasihi zilizoandikwa mfano hadithi lakini hazikulenga watoto wala vijana bali zilimlenga msomaji yeyote mfano kazi ya C.K Omari (1970) Hadithi za Bibi.
                                                                           3.
 ilipopitishwa sheria ya ndoa ndipo na watoto walianza kujulikana, lakini kujulikana huko hakukuendana na uandishi wa fasihi ya watoto na vijana. Hivyo kufikia miaka ya (1980) ndipo watoto walipoanza kutambulika na kupewa nafasi. Na kuanzia kipindi cha (1990)  kulikuwa na kuibuka kwa waandishi wa kazi ya kifasihi mfano kazi za Mulokozi kama Moto wa mianzi (1996), Ngome ya mianzi (1990), Ngoma ya mianzi (1991) Nyakiru Kibi na wengine pia kulikuwa na uanzishwaji wamradi wa  usomaji wa vitabu kwa watoto. Hii ikawa chahu kwa kuibua waandishi na kuanza kuandika kazi nyingi za watoto na vijana. Mfano Mwendo ya E. Lema (1998) kilichochapishwa na mradi wa vya watoto.
Baada ya kuangalia historia ya maendeleo ya fasihi ya watoto na vijana katika Tanzania sasa  tuangalie matatizo yanayoikumba fasihi watoto na vijana  nchini Tanzania. Fasihi hii inakumbwa na matatizo kama vile;
Maendeleo ya sayansi na teknolojia; kutokana na maendeleo haya fasihi ya watoto na vijana Tanzania wanao andikiwa hawako tiari kusoma fasihi hizo kutokana na kutumia muda mwingi katika kuangalia michezo kwenye runinga na mambo mengi hivyo kazi nyingi za waandishi zimekuwa zikikosa soko jambo linaloweza kusababisha hatari ya kupungua kwa waandishi wa fasihi ya watoto na vijana.
Ufundishwaji; fasihi ya watoto na vijana kwa kipindi kirefu sasa haijapata nafasi ya kufundishwa shuleni hadi vyuoni. Ndiyo maana waandishi  wengi wa mwanzo na hata leo hawajui muundo wa vitabu vya watoto na vijana ndiyo hata uandishi mwingi wa fasihi unakiuka mashariti hayo. Mfano ujenzi wa wahusika, uhalisia na mengine. Katika ujenzi wa wahusika kazi nyigi huonekana  kuwapa uhusika wasiofanana nao mfano. Abdul selemani katika fasihi ya Mpishi mwenye kibiongo (2000). Husababisha watoto kukosa haki ya kujifunza kazi zinazowalenga ambapo wale wenye vipaji wangepatika haraka na kuingizwa katika uwanja huu wa fasihi.
Waandishi; fasihi ya watoto na vijana mpaka sasa inaandikwa na watu wazima, watoto bado hawajapewa nafasi sana katika uwanja huu ambao unawahusu. Tukiangalia kazi zilizoandikwa
                                                                              4.

na watoto zitakuwa chache sana. Lakini tunawaona wandishi kama kina Mulokozi, Lema, B. Mtobwa nawengine, hawa ni watu wazima ambao wanaandika kazi za watoto.
Ukosefu wa uhalisia; kuna baadi ya kazi za fasihi zilizoandikwa kwa ajili ya watoto hazina uhalisia wa matukio yanayoweza kufanywa na watoto au vijana. Baadhi ya kazi hizo zikisomwa na watoto ni nivigumu kuelewa na ni vigumu kuamini au kuchukulia kuwa matukio yanayotendeka ni ya kweli, hivyo baadhi ya kazi hizo za fsihi zinatumia fantasia nyingi. Mfano Marimba ya Majariwa cha E. Semzaba (2008) Kalikalange mtoto wa ajabu na nyingine ya Charles kayoka.
Hakuna uhamasishaji wa usomaji vitabu kwa watoto. Tangu kuanzishwa kwa utaratibu au sheria ya usomaji vitabu kwa watoto, msisitizo haupo kiasi kwamba usomaji wa kazi hizi za fasihi umebakia kuwa wa lazima endapo mtu atatakiwa kufanya hivyo. Hata kwa watoto hakuna msisitizo wanaowekewa shuleni hata majumbani mwao. Hivyo ukosekanaji wa msisitizo wa usomaji utafikia kipindi waandishi watapunguza hamu ya kuandika fasihi hii kwani anyeandikiwa hayuko tiali kusoma.
Upungufu wa maktaba, katika nchi ya Tanzania zimekuwepo maktaba nyingi za vitabu mfano maktaba za shuleni, mikoa, taifa lakini hakuna maktaba ya vitabu ambayo ina vitabu vya watoto na vijana. Ukosekanaji huu unafanya watoto na vijana kushindwa  kujielimisha juu ya masula yanayowakabili kwani kazi nyingi za fasihi za watoto na vijana zinaelezea mambo yanayowakumba. Mfano fasihi za Zindera, mitego kabambe, sokoni kariakoo.
Mwitikio wa wazazi kuendeleza vipaji vya watoto na vijana wao. Hii tunaweza kuichukulia kama changamoto katika maendeleo ya fasihi ya watoto na vijana kwani kuna baadhi ya watoto huzaliwa na vipaji vya kuweza kufanya sanaa fulani mfano uimbaji mashairi, ubunifu wa usimiliaji na mengine lakini kutokana na kukosa ushirikiano na wazazi  wanashindwa kuonesha uwezo wao hivyo kigezo hiki kinaweza kuchukuliwa kama tatizo kwani waandishi wengine huzaliwa na vipaji.

                                                                             5.
Ugumu wa kuweka mipaka kati ya fasihi ya watoto, vijana na watu watu wazima. Ugumu huu umesababisha watoto na vijana kushindwa kujua ipi ni fasihi yenye kuwalenga na ipi haiwalengi. Hii imesababisha watoto kusoma hata fasihi zisizokuwa zao, japo sio jambo baya kusoma fasihi hizo.
Baada ya kupitia matatizo yanayokabili fasihi ya watoto na vijana, sasa ni wasaa wa kutazama njia za kutatua matatizo hayo.Katika kutatua matatizo yanayo ikabili fasihi ya watoto na vijana njia zifuatazo zinaweza kutumika ili kupunguza matatizo hayo.
Fasihi ya watoto na vijana iingizwe katika mtaala wa ufundishwaji, hii inaweza kuwaongeza motisha  kwa watoto na vijana kusoma fasihi kwani somo hilo litakuwa lalazima na kupitia usomaji huo tunaweza kupata waandishi wengi vijana au watoto kwani watakuwa na uelewa juu ya masuala ama ya kijamii, kiuchumi au kiutamaduni yanaowasibu na kuweza kuyaandika.
Kutoa kipaumbele kwa kazi bora za fasihi ya watoto na vijana. Mfano katika nchi zilizoendelea fasihi ambazo huonekana bora,  mwandishi hutunukiwa heshima kwa kazi yake nzuri. Hivyo utoaji huu wa zawadi au heshima juu ya kazi ya mwandishi inaweza kuongeza mwamko kwa waandishi na kukuta wakiandika kazi zenye sifa za kuitwa kazi za  watoto na vijana kuliko kuandika bila kuzingatia hadhira lengwa.
Serikali itambue mchango wa fasihi ya watoto na vijana na kuanzisha maktaba za vitabu vya watoto na vijana kama zilivyo maktaba zenye vitabu vya watu wazima.
Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa fasihi ya watoto na vijana ni fasihi muhimu kama zilivyo fasihi nyingine tena ni fasihi iliyobebe ujumbe mzito unaolenga kukomboa jamii ya watoto na vijana kutoka katika baadhi ya mira potofu mfano mzuri ni fasihi ya Zindera ya E. Sabun pamoja na nyingine.


                                                                           6.

                                                             MAREJEO.
Bruno (2011) Social Issues in Contemporary African American Young Adult Ficton:
                         Iliyopakuliwa  kutoka http://is.muni.cz/th/183848/pedf_m/social
                         issues_in_contemporary_african_american_young_adult_fiction.pdf
Children’s Literature: http://en.wikipedia.org/wiki/children’s_literature
Kateta Mwana Charo (1976) Toka Kizazi Hadi Kizazi. Ndanda Enterprises: (T) Ltd.
Olua, O. S. Victor et al (2002) Children Abuse and Neglect. Women’s Aid Collective:
                       iliyopakuliwa kutoka
                        saa 7:30 mchana.
TUKI (2004) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (Toleo la 2). Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Young Adult Library Service Association (YALISA) (2011) Young Adult Fiction: iliyopak
                         Kutoka  www./en.wikipedia.org/wiki/young_adult_fiction Iliyosomwa tarehe 20- 05- 2012. saa 7:32 mchana.




                          



                                       BARUA ZA SHAABAN ROBERT

Katika mjadala huu tutaanza na utangulizi ambao unajumuisha maana ya Barua na muhtasari wa Kitabu cha Barua za Marehemu Shekhe Muheshimika Shaaban Robert,katika kiini tutachambua fani na maudhui katika barua hizo na tutamaliza kwa hitimisho la mjadala mzima.

TUKI (2004) wanasema barua ni maandishi yenye ujumbe yanayopelekwa kwa mtu mwingine kwa njia ya mkono au kupitia posta.Kwa jina lingine huitwa waraka.

Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, mfumo huu wa barua umeathiriwa kwa kiasi fulani na kupoteza washabiki wa kutumia njia hii ya mawasiliano na kuibuka njia nyingine zinazorahisisha mawasiliano kama barua pepe.

Kitabu cha mkusanyiko wa barua za Shaaban Robert ni kitabu chenye mkusanyiko wa barua zililimbikizwa kwa miaka mingi na Bw Yusuf Ulenge ambaye ni mdogo wake Shaaban Robert.

Kwa nasaba Yusuf Ulenge na Shaaban Robert ni watoto wa mama mmoja ila baba mbalimbali, baada ya mama Yusuf kuachwa na Baba wa Shaaban Robert anaolewa na baba yake Yusuf. Haikuwa vigumu kwa Yusuf kulelewa na Shaaban Robert.

Barua za marehemu Shaaban Robert ni mkusanyiko wa barua ambazo Shaaban Robert alikuwa akimwandikia mdogo wake Yusuf Ulenge kati ya mwaka 1931 na 1958.Barua hizo zilihifadhiwa kwa zaidi ya miaka 50 na hata zikaweza kupatikana na kuchapishwa katika kitabu hiki mnamo mwaka 2000 na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Kitabu hiki pia kimekusanya nyaraka nyingine za Shaaban Robert alizokuwa anaandika katika gazeti la mamboleo katika kipindi cha ukoloni Tanganyika.

Barua hizi ziligundulika mwaka 1993 wakati watafiti wa TUKI, M.M Mulokozi  na T.Y Sengo wakiongozana na marehemu Mwalimu Pera Ridhiwani na Salumu Ali Kibao walipokuwa wakifanya utafiti wa historia na maendeleo ya ushairi wa Kiswahili mkoani Tanga. Watafiti hao walibahatika kukutana na kumuhoji mzee Yusuf Ulenge nyumbani kwake Chanika Handeni tarehe 4.9.1993 na katika mahojiano naye aliwakabidhi jarada lenye barua hizi pamoja na picha na nyaraka nyinginezo.Kutokana na sababu mbalimbali barua hizo hazikuweza kuchapishwa kwa kipindi hicho.

Ufuatao ni uchambuzi wa fani na maudhui katika kitabu hiki,kwa kuanza na uchambuzi wa kipengele cha maudhui.

Maudhui ni dhana pana inayoweza kuelezwa kwa jinsi mbili ambazo kimsingi zinahusiana.Jinsi ya kwanza,maudhui ni jumla ya masuala au mambo yanayoshughulikiwa katika kazi ya kifasihi. Masuala haya hutokana na jinsi mtunzi au mwandishi anavyoikuza mada ambayo ni msingi wa utunzi wa kazi yake na jinsi ya pili ni hutumia maudhui kukirejerea kiwango cha kimaana (Wamitila:2003).

Maudhui huundwa na vipengele kadhaa ambavyo ni dhamira, migogoro, ujumbe, msimamo na falsafa.

Dhamira.Dhamira ni lengo au shabaha ya kazi ya fasihi (Njogu na Chimela:1999). Dhamira ni kipengele mojawapo cha kazi ya fasihi, mara nyingi huwapo na dhamira kuu ambayo hasa ndiyo kiini cha kazi ya fasihi.

Dhamira kuu katika barua hizi za Shaaban Robert ni ukombozi, ukombozi ni hali ya uokoaji wa watu kutoka kwenye hali mbaya ya udhalimu au hali duni.Hali hiyo imejitokeza katika barua hizo, kwani Shaaban Robert ameonesha dhamira ya ukombozi wa kijamii,kisiasa,kiuchumi na kielimu.

Ukombozi wa kijamii umejitokeza katika barua nyingi alizoziaandika Shaaban Robert ambazo zilisisitza masuala ya kijamii kama Utu wema, maadili, uwaminifu na mapenzi na ndoa.Pia amesisitiza jamii kuwa ushiriakiano ktika masuala mbalimbali ya kijamii kama vifo.

Pia mwandishi ameonesha dhamira ya ukombozi wa kisiasa kwa kusisitiza umoja na mshikamo katika kupigania uhuru na umuhimu wa uhuru katika nchi.Pale alipoandika katika waraka na ii.13 “WAINGEREZA WATASHINDA

Mungu nipe buruhani,                                                                                                                          

Unibakishe mwakani,

Niadhmishe amani,

      Na wenzangu mahuria.

Ukombozi wa kiuchumi,hali hii imejitokeza katika barua alizoandika  Shaaban Robert alipokuwa anamjulisha Yusuf kuhusu shughuli ya uvuvi anaofanya Jaffari na taarifa ya hali ya anguko la uchumi duniani na kusababisha ongezeko la kodi.Mwandishi alisisitiza jamii ijitume katika uzalishaji ili kuepuka utegemezi na umaskini unaotokana na anguko la kiuchumi katika mataifa makubwa.Mfano barua namba 14.Pia mwandishi ameonesha alikuwa anapenda kuwasaidia ndugu zake kwa hali na mali ili awainue kiuchumi.Mfano barua namba 26,ila barua hii mwandishi amekosea hesabu kwani pesa iliyotolewa ni shs 65/- na mchanganuo wake jumla ni shs 75/-.

Ukombozi wa kielimu,hii ni dhamira iliyojitokeza katika barua nyingi za Shaaban Robert,hali hiyo inaonesha namna mwandishi alivyokuwa anazingatia elimu na kuitilia mkazo kwa kumsisitiza Yusuf Ulenge kwa kiasi kikubwa pindi wanapowasiliana kwa barua.Wazo hilo lilikuzwa kwa njia zilizowazi kwa mfano katika barua ya kwanza (1), tatu (3), nne(4), tano (5), sita(6) na waraka wa 22 mwandishi anaonekana kumtumia mahitaji muhimu ya shule kama vile kalamu,penseli,fedha za ada na kujikimu na kumsisitiza kuwa mchapa kazi na mwenye nidhamu katika kipindi chote cha maisha.Pia alimshauri Yusuf aachane na masuala ya mapenzi na ndoa na azingatie elimu kwanza.Hivyo mwandishi ameonesha kuwa elimu ni muhimu katika maisha na jamii kwa ujumla.

Kwa mfano: Barua ya tano(5)   Nimekuletea kitabu kidogo cha ngozi pamoja na                          

                                                     kalamu,yaan,zawadi yako

                     Barua ya pili(2)      Leo nafurahi sana kukuletea  zawadi vitabu viwili na kitamba leso kimoja.Baada ya kazi zako za skuli au chuoni nataka uzidi kujikaramisha kuandika katika vitabu hivi

Kutokana na dhamira kuu tunaweza kubainisha dhamira nyingine ndogondogo ambazo zimejitokeza katika barua hizi. Dhamira hizi ni kama zifuatazo:-

Mapenzi ya kweli.Katika barua hizi mwandishi Shaaban Robert anaonesha mapenzi ya kweli kwa ndugu zake kwa kuwajali,kuwatunza,kuwashauri na kuwajulia hali kila mara ambapo anapata nafasi. Pia anaonesha kuwa alikuwa na mapenzi ya dhati kwa mke wake.

Kwa mfano katika barua ya 61.

“Bibi Amina alikuwa na mimba pevu ilikuwa si wajibu wangu kuondoka kabla ya kujifungua”

Barua ya 8.

Sifurahii Yussuf mwanangu, kuwa tangu uanze kupokea masomo hujaniandikia bado habari za maendeleo yako ba tabu zako

Pia Yusuf alionesha mapenzi ya kweli kwa kaka yake Shaaban Robert pale alipoumia mkono wa kulia na kuweza kumuandikia barua kwa mkono wa kushoto.

Kwa mfano barua ya 35.

barua yako nimepata.Nasikitika kusoma ndani yake kuwa u mgonjwa wa mkono.Hakika ni mapenzi makubwa yaliyokufanya hata kuniandikia kwa mkono wa shoto”

Mapenzi ya kweli kwa mama yake Shaaban Robert. Shaaban Robert alikuwa na mapenzi ya dhati kwa mama yake kiasi kwamba aliweza kumuita mtoto wake jina la mama yake.

Kwa mfano katika barua ya 61.

alijifungua November 28 1940 mtoto wa kike nimemuita Mwanamwema kwa kumuheshimu mama yangu

Pia Shaaban Robert ameonesha ana mapenzi ya kweli kwa nchi, mji na jamii yake nzima.Mfano barua ya 14.

“……….matumaini kwamba hutasahau kuinua juu jina la ukoo wako na nchi uliozaliwa.”

Maadili mema.Maadili ni mwenendo mwema,maonyo au mafundisho yatolewayo na mtunzi wa kazi ya fasihi.Dhamira hii imejitokeza kwa mwandishi Shaaban Robert anamsisitiza mdogo wake kufuata maadili mema kwa kutotumia matusi, kutoondoka shule bila ruhusa.

Kwa mfano barua ya 2.

sitaki uandike ndani ya vitabu neno lolote baya namna ya matusi

huna haja ya kuja huku iwapo hukupata ruhusa ya wakuu wako

Halikadhalika Shaaban Robert anaonekana kama mtu mwenye hekima na maadili kwani kila mara alikuwa akijaribu kumsisitiza mdogo wake kuwa na maadili mema.

Uaminifu na utu,ni hali ya kuwa na tabia zinazolingana na hadhi ya mtu na mwenye huruma juu ya matatizo ya wenzako inayokufanya ukubalika jamii nzima.Suala hili limejitokeza katika barua  za Shaaban Robert ,anaendelea kumsisitiza ndugu yake juu ya utu na uaminifu katika maisha.

Kwa mfano barua ya 5

“………… ndugu yangu ufuate maisha bora ya juu uishi duniani uweze kusaidia watu mwisho yako uweze kusema bila hofu kuwa sikumliza mtu ila nilishawasaidia

Umuhimu wa kuweka akiba. Katika barua hizi, barua ya 25 na 60 mwandishi Shaaban Robert anamsisitiza mdogo wake juu ya kujiwekea akiba ili iweze kumsaidia pindi apatapo matatizo ya ghafla.Suala hili linaigusa jamii yetu kwani kuweka pesa benki kuna kuepusha mtatizo mengi kama ya ujambazi na pesa kupotea au kutumia bila ya mpangilio.

Barua ya 60.

shauri langu juu ya kuweka fedha ya akiba ni kufungua hesabu katika Post Office Serving Bank

Umoja na mshikamano.Shaaban Robert alikuwa anapenda umoja na mshikamano kwa ndugu zake na wananchi kwa sababu alikuwa napenda kushirikiana na wenzake na ndiyo maana aliandika barua ya kuomba uanachama katika chama cha wakulima.

Waraka na.ii. 2.

kama kuingia kwa wanachama katika chama chenyewe bado kufungwa tafadhali na mimi nifanye mwanachama

Nafasi ya mwanamke.Katika barua hizi zinamchora mwanamke kama mlezi,nafasi hiyo ni muhimu sana katika jamii hususani mwanaume anapokuwa mbali na familia yake, hali hii imejitokeza pale Shaaban Robert alipomjulisha Yusuf Ulenge kuhusu taarifa alizopata juu ya maradhi ya mwanae kutoka kwa mke wake.

Barua ya 29.

leo hii nimepata barua itokayo kwa mke wangu kuniarifu kuwa mtoto mgonjwa sana kuwa hospitali zimeshinda

Pia ameonesha kuwa mwanamke ana haki ya kumiliki mali katika jamii. Hali hiyo imejitokeza pale alipomjulisha Yusuf  kuwa amenunulia Mwanjaa shamba.

Barua ya 47

“nimemnunulia miss Mwanjaa kijishamba kwa shs. 400/=”

Suala la ndoa.Katika barua hizi suala la ndoa limejitokeza kwa kutuonesha hatua zinazopitiwa kabla ya kufunga ndoa na uvumilivu katika ndoa.Shaaban Robert alimjulisha Yusuf kuhusu kaka yake Mwishehe Ulenge kuwa ametoa posa.Pia alimsaidia Yusuf kuhusu kutoa posa pindi alipotaka kuoa.Posa ni barua inayotumwa kwa wazazi wa mwanamke kwa lengo la kuoa binti wao fulani.

Barua ya 38.

kaka yako Mwishehe Ulenge aliposa Zuhura binti Mkindi

Pia Bw Yusuf alijulishwa habari za ndoa za jamaa zake mbalimbali.

Barua ya 33.

Mwajuma na Mwasalama binti zake Rajabu wameolewa

Dhamira hii ilijitokeza pia kwa Yusuf pindi alipopendana na binti wakati bado yupo kwenye masomo lakini Shaaban Robert alimshauri aendelee na shule suala la ndoa litakuja baada ya kusoma na kuwa na maisha yako ya kujitegemea.

Suala la kifo,Ni dhamira inayojitokeza sana na kuonesha masikitiko makubwa kwa Shaaban Robert. Kifo ni jambo linaloleta huzuni kwa jamii hususani wahusika wanaohusika moja kwa moja.Shaaban Robert alifanikiwa kumjulisha Bw Yusuf vifo mbalimbali vya ndugu na jamaa vilivyokuwa vinatokea na kuonesha majonzi makubwa.

Barua ya 33.

ila nasikitika kuandika barua ya kifo cha Bw Ali Bin Khamis, maarufu, Ali wa kadhi



Barua ya 37.

nasikitika sana kukutangazia kifo kwa kufa maji cha ndugu yangu Abdallah Robert

Barua ya 40.

“…misiba iliyotokea kwetu ni ya Mamiepesa na Mr Itela Mwajalimu

Alipenda kutoa taarifa za kifo na kuonesha huzuni kwa jamii kama njia ya kuonesha umoja na ushirikiano. Kati ya mikasa ya Shaaban Robert ambayo imemuhuzunisha sana ambayo haielezwa katika diwani yake ya Maisha yangu na Baada ya Miaka Hamsini ni kifo cha mwanaye aitwaye Kihere.

Barua ya 35.

nahuzunika mno kukutangazia kifo huko Tanga cha mtoto wangu mchanga .K.G. Robert.”

Migogoro.Ni dhana inayojitokeza katika kipengele cha maudhui.Mgogoro ni hali ya kutokuafikiana baina ya pande mbili au zaidi, fujo( TUKI:2004). Fasili hiyo inajitosheleza kwani migogoro huweza kuwa hali ya kutoelewana au kutokubaliana. Dhana hii inajitosheleza katika barua hizi za Shaaban Robert.Mwandishi ameonesha migogoro ya namna tofauti kama mgogoro wa kinafsiya,mgogoro wa kijamii, mgogoro kati ya wazo na wazo,falsafa, na baina ya hali na hali na mgogoro kisiasa.

Mgogoro wa kinafsiya,mgogoro huu ujitokeza katika nafsi ya mhusika ambao huweza kusababishwa na jamii.Mgogoro unajitokeza kwa Shaaban Robert pale alipokuwa analalamika juu mvutano uliotokea katika jamii yake kisa mwanaye na kufikia kuliita ujinga.

Barua ya 34. “Jambo la kijinga na la kustusha………….”

Mgogoro huu, pia umejitokeza katika barua namba 15 pale aliposita kumweleza Yusuf matatizo ya kifamilia aliyokumbana nayo alipokuwa Tanga.

Barua ya 15. “Sipendi kuharibu utamu wa barua hii kwa kukueleza mikasa nilioipata…”

Mgogoro wa kijamii,Shaaban Robert alimjulisha Yusuf migogoro mbalimbali iliyojitokeza katika jamii yao.Migogoro iliyojitokeza ni ya kijamii, pale familia ya Shaaban Robert iliposigana kutokana na jina la mtoto Kihere.

Barua ya 34.

ziada kwetu kuna machafuko sana ziko sehemu mbili za washindani. Wamkataao Kihere na wamtakao Kihere

Vilevile kuna mgogoro unaotokana na suala la ndoa. Mgogoro huu ulisababisha wanandugu kupigana na kumuumiza dada yao.Barua ya 31.

wamepigana na kuhasimiana sana sana. Dada yao wamemchana visu masikini

Mgogoro mwingine ni kati ya wazo na wazo,falsafa, na baina ya hali na hali.Mgogoro huu umejitokeza pale Shaaban Robert alipopinga wazo na maamuzi ya ndugu zake la kumrudisha fedha wakati alituma fedha hizo kwa ajili ya kununuliwa nazi. Barua ya 36.

umeandika barua ya kurudishiwa fedha hii ni kwa sababu eti hakuna mnazi Tanga. Ajabu gani hii?”

Mgogoro wa kisiasa, huu ni mvutano kati ya pande mbili zinazosigana kuhusu masuala ya kisiasa.Mgogoro huu pia umejitokeza katika Waraka na.ii.13 “Waingereza Watashinda” katika waraka huu unaonesha kuna mgogoro kati ya wananchi wa Tanganyika na Wakoloni kuhusu suala uhuru,pia kuna mgogoro kati ya wananchi wa Tanganyika wenyewe ambao wanapenda uhuru na wasio penda uhuru.

Kila mpinga uhuru,

Atafuta kujidhuru,

Mungu hatamwamuru,

             Kuwa juu ya dunia.



Ujumbe. Ujumbe ni neno ambalo humaanisha taarifa aipatayo msomaji asomapo kazi ya kifasihi. (Wamitila:2004). Hivyo ni dhahiri usomapo barua hizi ni lazima msomaji apate ujumbe husika. katika kitabu hiki cha mkusanyiko wa barua za Shaaban Robert tunapata ujumbe mbalimbali kama vile:-

Elimu ndiyo ufunguo wa maisha, barua hizi kwa kiasi kikubwa zilikuwa zinamsisitiza Yussuf kuzingatia elimu na kuwa mwenye juhudi ili aepuke mazingira ya ujinga katika maisha.

Mfano barua ya 22

ni jambo zuri kujifunza kuaridhi masomo kwa moyo kuliko kusoma kutupilia mbali

Wema ni hazina.Shaaban Robert alimsisitiza Yussuf kuwa mwema na mwenye nidhamu kwa ndugu na jamaa hata kwa walimu wake.Jambo hili linatufunza kuwa kwa jamii yetu ili tuishi kwa amani na utulivu.

Akiba haiozi.Shaaban Robert anatufundisha kuwa tukumbuke kuweka akiba katika benki kwa ajili yetu wenyewe.Pale alipomkumbusha Yusuf kufungua akaunti.

Mapenzi na masomo ni vitu ambavyo haviendani.Shaaban Robert anaitahadharisha jamii kuwa elimu kwanza na ukishafanikiwa ndiyo ujiingize katika masuala ya mapenzi na ndoa pale alipomkataza Yusuf kujiingiza katika masuala ya ndoa kabla hajamaliza masomo.

Kutoa ni moyo na wala siyo utajiri.Katika barua hizi Shaaban Robert anatuonesha kuwa kumsaidia mtu ni jambo la umuhimu katika jamii kwani aliweza kuwasaidia ndugu na jamaa kwa nyakati tofauti na wala hakuzingatia kujilimbikizia mali.Mfano barua ya 26.

Msimamo.Dhana hii hutumiwa kuelezea mitazamo na mikabala sambamba na hali za kijamii, kisiasa na kiuchumi katika jamii zao. (Wamitila:2003). Katika kitabu cha mkusanyiko wa barua za Shaaban Robert ameonesha kuwa anamsimamo wa kiyakinifu kwa kuhitaji jamii kubadilika na kuwa waaminifu na wema, wachapakazi na wenye bidii katika elimu ili kuendana na maendeleo ya jamii.

Mtazamo.Ni namna mwandishi au mtunzi wa kazi ya fasihi anavyoyachukulia mambo, katika kitabu hiki mwandishi Shaaban Robert anaonesha kuwa ana mtazamo wa kimapinduzi kwani anaeleza mambo yaliyotokea na yaliyopo katika jamii ya sasa na kupigania mabadiliko kupitia elimu ili kuwa na jamii yenye nidhamu na maadili mema katika masuala kama uzalendo,mapenzi na ndoa.

Falsafa.Hii ni dhana inayotumiwa kuelezea mwelekeo wa kimawazo ambao unadhihirika katika kazi ya kifasihi (Wamitila ameshatajwa).Falsafa ya kazi ya fasihi inatakiwa ichambuliwe kwa kuzingatia jinsi kazi inavyoutazama ulimwengu.Hivyo katika kitabu hiki cha Barua za Shaaban Robert,falsafa ya mwandishi ni maadili mema, juhudi na nidhamu ndiyo msingi wa maendeleo katika masuala mtambuko.

Licha ya kuwa na vipengele vya maudhui vilivyojitokeza katika barua hizi za Shaaban Robert, pia kuna vipengele vya fani vilivyojitokeza.Fani ni ule ufundi wa kisanaa anaotumia msanii katika kazi yake (Senkoro:2011).Fani hujumuisha vipengele mbalimbali ambavyo ni:-

Muundo.Muundo ni jinsi kazi inavyoonekana na uhusika umbo lake. Msomaji anapaswa kuzingatia mpangilio wa matukio(Wamitila ameshatajwa). Katika kitabu hiki cha mkusanyiko wa barua za Shaaban Robert katika barua zake hizo zote zilikuwa na muundo wa moja kwa moja kwani aliweza kupanga matukio kimantiki ndani ya barua na pia barua zimepangwa kwa mtiririko mzuri unaoweza kuhusisha matukio.Barua zinazoonesha Yusuf yupo shuleni mpaka akifanya kazi baada ya kumaliza masomo yake.Pia mwandishi ametumia miundo tofauti ya barua.Miundo iliyotumika ni muundo wa barua za kirafiki kwa kiasi kikubwa,muundo huu hujengwa kwa anuani moja ya mwandishi ambayo hukaa juu upande wa kulia.Mfano barua namba (1), (2), (12), (14), (40), (37).Pia kuna barua za kikazi/kiofisi zenye anuani mbili,moja upande wa kulia ni anuani ya mwandishi na ya pili ni upande wa kushoto ni anuani ya mwandikiwa kama vile barua namba (45, (49), (69)).Muundo mwingine ni barua za gazetini, muundo wa barua hizo ni tofauti sana barua nyingine kwani ina anuani moja ya mwandishi inayokaa chini upande wa kulia.Mfano waraka ii.8 na 7.

Pia muundo wa mashairi.Katika kitabu cha Barua za Shaaban Robert ni kuwa si kila mshororo unajitosheleza kimaana,ipo inayojitosheleza na isiyojitosheleza.Mishororo ya shairi la “waraka” namba II:16. Shairi la “Mapenzi” lina vipande viwili lakini kila shairi la waraka namba II:13 na II: 11 zina ubeti wa mishororo minane.Pia mshairi amefanikiwa kuzingatia vina kuliko mizani.

Kwa mfano:-  waraka namba II:13

            “kila mpinga uhuru”

            “Atafuta kujidhuru”

            “Mungu hatamwamuru”
            “kwa juu ya dunia”

Waraka wa II:16.

            “dunia mambo sasa,hayashindi mapenzi”

            “Kati ya hizo anasa,mapenzi ni azizi”

“Si jambo la kupapasa, kweli kupu waziwazi”
“Yamethibitika hasa, kama ni hitaji la enzi”
“Ni shina kabisa, chimbuko la ukombozi.”
“Kuadi hatakasa, na kuyafuta machozi”


Mtindo.Katika kazi ya fasihi ni ile namna ambayo msanii hutunga kazi hiyo na huipa sura ambayo kifani na kimaudhui huainisha kanuni au kawaida zilizofuatwa kama ni zilizopo (za kimapokeo) au ni za kipekee(Senkoro:2011).Hivyo mtindo ni njia sahihi ya kuonesha na hata upekee wa mtungaji wa kazi husika.Katika kazi hii Shaaban Robert amefanikiwa kutumia nafsi zote tatu katika barua zake nyingi.Nafsi ya msanii ijitokezayo katika barua hizi ni nafsi ya kwanza umoja ambayo ndio imejitokeza kwa kiasi kikubwa kushinda nyingine. Pia amefanikiwa kutumia nafsi ya pili na ya tatu katika kufikisha ujumbe.

Pia msanii amefanikiwa katika kuonesha upekee katika barua hizo kwa kutumia mtindo wa barua za kirafiki, barua za kiofisi.Vilevile mtindo wa insha,mtindo wa kishairi na mtindo wa barua za gazetini uliojitokeza katika barua alizokuwa anatuma kwenye gazeti.

Barua nyingi alizoandika Shaaban Robert ameonesha upeke wa mtindo kwa uwezo wake wa kuchanganya lugha ya Kiswahili na Kiingereza.Mwandishi alitumia lugha zote za Kiswahili na Kiingereza na kuonesha umahiri wake katika lugha lugha hizo.

Kitabu cha Barua za Shaaban Robert kina mtindo wa ufafanuzu wa barua.Katika kila mwisho wa barua kuna maelezo yanayofafanua kwa ufupi barua husika pamoja na tanbihi inayowahusu hasa wahusika waliojitokeza katika barua.

Vilevile katika kitabu hiki kuna upekee wa mtindo kwa kutumia picha,kwani kuna picha mbalimbali ambazo zimeambatanishwa katika kitabu hiki zinazosawiri wahusika waliomo.Mfano ukurasa wa (96), kuna picha ya Yusuf Ulenge, uk(147) kuna picha Mzee Yusuf Ulenge na familia yake,Chanika Handeni,Februari 2002, uk(43) kuna picha Shaaban Robert uzeeni, uk(49) kuna picha ya kaburi la Shaaban Robert.Pia kuna picha za watoto wa Shaaban Robert.

Wahusika.Katika kazi ya fasihi kuna wahusika wa aina mbalimbali,wahusika hao waweza kuwa watu au viumbe wenye shaba ya kuwakilisha mawazo au tabia za watu au viumbe.Katika barua hizi wahusika waliojitokeza ni watu ambao ni Shaaban Robert pamoja ndugu na jamaa zake.

Katika maandishi haya mhusika  mkuu ni Shaaban Robert ambaye alikuwa mfanyakazi wa forodha,ni mtu mwenye kupenda kuwasaidia ndugu na jamaa kupitia kipato chake alichokipata hivyo jamii yake ilimtegemea sana kiuchumi,pia Shaaban Robert anaonekana kama mtu mwenye kupenda masomo kwa kumsisitizia mdogo yake(Yusuf) azingatie masomo na awe mwadilifu na tunaona jitihada zake za kujiendeleza kimasomo.Mhusika huyu ameonesha uzalendo na umuhimu wa uhuru katika barua yake aliyoiandika kwa mtindo wa ushairi.

Mhusika mwingine ambaye anajitokeza tangu mwanzo kama siyo mpaka mwisho mwalimu Yusuf Ulenge ambaye ni ndugu wa karibu wa Shaaban Robert.Kwa hiyo Yussuf Ulenge ni mhusika ambaye ni hai katika ulimwengu kwasababu anawakilisha dhana au mawazo ambayo ni muhimu kuyazingatia kama elimu, kuwa na bidii na kuwa mtu mwema.

Wahusika wengine ambao wanajitokeza katika barua hizi ni Amina Kilenge ni mke wa Shaaban Robert,Kilenge ni mtoto wa Shaaban Robert ambaye alifariki baada ya siku 33 tokea kuzaliwa kwake,Ali wa Kadhi ni rafiki wa Shaaban Robert,Alfonso ni mwalimu wa Yussuf na wengine wengi kama Mwinshehe, Jaffari,Mworongo, Mwanjaa na jamaa wa karibu wa Shaaban Robert.

Mandhari.Hiki ni kipengele muhimu katika kazi ya fasihi,hiki ni kipengele kingine cha fani katika uchambuzi.Mandhari huweza kuonesha uhusiano na vipengele vingine vya kazi husika. Katika barua hizi mandhari iliyotumika ni yakinifu na halisi inayosawiri dhamira husika pamoja na wahusika. Kwa mfano mwandishi amemuonesha Yusuf yupo Old Moshi wa kati Shaaban Robert alikuwa akifanya kazi forodhani.Kwa kiasi kikubwa katika barua hizi kuna mchanganyiko wa mandhari kama vile Dar es salaam,Kwake,Kisiu,Tanga ambako ni maeneo halisi ya Tanganyika kwa hivyo mandhari imefanikisha kuonesha kipindi husika cha miji na maendeleo yaliyokuwepo.Mandhari ya kitabu hiki yanaonesha kipindi cha ukoloni kwa kuonesha shule zilizokuwepo na mazingira aliyofanyia kazi Shaaban Robert.

Matumizi ya lugha.Lugha ni nyenzo muhimu sana katika kazi ya fasihi,maudhui na dhamira ya kazi ya kifasihi hutegemea lugha kufanikishwa na kuwafikia wasomaji.Hata mwandishi Shaaban Robert ametumia lugha kwa ubunifu ili kufanya kazi ipendwe na msomaji.Katika matumizi ya lugha hujumuisha vipengele mbalimbali ambavyo ni kama vile;-

Tamathali za semi.Hizi zina nafasi kubwa sana katika kufanya kazi ya fasihi ivutie iwe na msisitizo na mnato mkubwa.Katika kitabu hiki kuna tamathali za semi mbalimbali ambazo zinajotokeza ambazo ni kama vile:-

Tashibiha.Tashibiha ni ulinganishi wa moja kwa moja hutumia viungo au viunganishi. Katika barua hizi za Shaaban Robert tashibiha imejitokeza katika barua ya 30.

Tango bivu hubonyea kama embe

Twaa kisu ulikate kama papai kwa miraba

Vipande vidogo mithili ya mua                

Sitiari. Ni ulinganishi wa vitu mbalimbali bila kutumia kiunganishi. Sitiari katika barua hizi imejitokeza katika waraka II:7

tabia bora ni johari

Taashira.Hii ni aina ya sitiari ambayo itajapo sehemu tu ya kitu hapohapo sehemu hiyo huashiria au kuwa kuwakilisha kitu hicho.

Kwa mfano; johari huashiria kitu kizuri cha thamani ya juu.

Kejeli au kinaya.Hii ni tamathali ambayo maneno yake huwa kinyume kabisa na maana inayotakiwa kutolewa.Tamathali hii imejitokeza katika barua ya 36.

Hakuna cha bure kwa sisi masikini ambao ni wageni na ambao hatuna mnazi Tanga?”
wakati si kweli kuwa Shaaban Robert alikuwa maskini,mgeni wala mtu asiye na minazi huko kwao.

Lakabu ni jina la kupanga ambalo linaakisi nasaba yako,tabia,matendo au mwenendo wako. Katika barua ya 36 tamathali hii imejitokeza pale ambapo Yusuf alijiita jina la mshauri lakini Shaaban Robert aliona kuwa jina hilo linamfaa yeye.

katika barua yako nyingine umejiita mshauri

    Daraja yako ya kuwa mshauri ingefaa zaidi yangu kulingana na matendo yako

Vipengele vingine muhimu katika matumizi ya lugha ni kame vile methali, misemo na nahau. Vipengele hivyo hupamba na kupendezesha lugha katika kazi ya fasihi na kuipa upekee fulani.

Misemo ni maneno yanayotumika mara kwa mara kama yalivyo katika mazingira maalumu na kuleta maana maalumu.Kwa mfano katika barua ya 15.

ving’aavyo vyote si dhahabu

Barua ya 7.

Bora ndiyo itoshayo katika maisha

ndiyo mpenzi wa milele

Waraka wa II:9

Talaka si mke wangu

Kiasi kwa kiasi ni upiganaji lakini wema kwa maasi ni uungwana

Mwisho wa ghafla ni majuto

Ukijua kuoa na kuacha ujue

Nahau ni msemo uliojengwa kwa kutumia maneno ya kawaida lakini ambao huwa umesitiri maana tofauti na ile inayobebwa na maneno hayo katika matumizi ya kawaida.Kwa mfano barua ya 15.

Nimuukata usingizi

Methali ni kauli au tungo fupi yenye kubeba ujumbe mzito au mawazo mazito yenye kutokana na uzoefu wa jamii fulani. kwa mfano barua ya 30.

La mkata haliiti

Jogoo la shamba haliwiki mjini

Uteuzi na mpangilio wa maneno.Uandishi wa kifasihi unahusu matumizi ya maneno na mpangilio wa maneno hai yaliyoteuliwa.Katika barua hizi mwandishi ametumia lugha nyepesi na yenye kueleweka kwani msamiati wake kwa kiasi kikubwa unaeleweka wazi ingawa kuna matumizi ya msamiati wa lugha ya kiingereza kama barua ya 34 ametumia maneno kama dear, Government primary school, please see.

Pia kuna barua ambayo mwandishi ametumia lugha ya Kiingereza kwa mfano barua ya 44. Hivyo inaonesha wazi kuwa mhusika ambaye ni Yusuf Ulenge alikuwa ameshapevuka kielimu kutokana na kutumiwa barua zenye mchanganyiko wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.Vilevile unaweza kujua kiwango cha ujuzi wa lugha ya Kiingereza kwa mwandishi wa barua hizo.

Kwa kuhitimisha, kitabu hiki kimeonesha umahiri na ufanisi wa Shaaban Robert kwa kuweza kutunga barua kwa mitindo mbalimbali kama mtindo wa ushari.Pia barua hizo zimeonesha namna Shaaban Robert alivyokuwa mtu mwema, mwajibikaji, mwenye kuwathamini ndugu na jamaa  na kuwasaidia kwa hali na mali na anayeshikamana na masuala ya dini.Vilevile barua hizi zimeonesha masuala mazito ambayo hayakuoneshwa katika tawasifu zake.







MAREJEO

Mulokozi, M.M (2006) Barua za Shaaban Robert 1931-1958.Dar es Saalam:Taasisi ya

                      Uchunguzi wa Kiswahili:Chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Senkoro, F.E.M.K (2011) Fasihi.Dar es salaam:KAUTTU.

 TUKI (2004) Kamusi ya Kiswahili sanifu. Kenya: Oxford university press L.T.D              

Wamitila, K.W (2003) Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: English Press.

Wamitila, K.W (2004) Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Andishi. Nairobi: focus publications

                       LTD.

No comments:

Post a Comment